JamboMail.com – Burudani, Makala, Michezo, New Music, Mambo 10 & Lifestyle

The most read Swahili entertainment website in Tanzania, East Africa.

Nyimbo 10 za Bongofleva alizoimbiwa Wema Sepetu

Nyimbo 10 za Bongofleva alizoimbiwa Wema Sepetu

Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu anauza sana kwenye Bongofleva, kwa miaka wasanii wamekuwa wakipigana vikumbo kutaja jina lake kwenye nyimbo zao, inaonekana ni bidhaa unayouzika kwa urahisi katika soko la muziki.

Wema Sepetu Bongofleva

Utakumbuka katika historia ya shindano la Miss Tanzania, Wema Sepetu ndiye Miss aliyeandikwa na kujadiliwa sana na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa muda mrefu zaidi.

Soma pia Video 10 za bei ghali zilizowahi kufanyika Bongo

Sio waimbaji maarufu tu wa Bongofleva kama Diamond Platnumz, Alikiba na Harmonize, bali hata wasanii wa Hip Hop kama Fid Q, Joh Makini na Roma wanajua nguvu ya Wema Sepetu na ndio sababu ya kumtaja katika nyimbo zao kama ifuatavyo;

  1. Diamond – Nimpende Nani (2012)

Staa huyu wa WCB Wasafi ambaye amewahi kuwa na uhusiano na Wema miaka ya nyuma, amemtaja mrembo huyo katika nyimbo zake tatu, Kesho (2012), Fire (2017) na Nimpende Nani (2012) ambao ndio kamzungumzia sana.

“Yasiwe kama ya Wema Sepetu kila siku magazeti, ajue nidhamu na mila ya kwetu mjuzi kupetipeti…. Mpole kama Jokate, ila sauti kama Wema akiwa analia kicheko kama cha Fetty,” Diamond katika ngoma, Nimpende Nani kutoka kwenye albamu yake ya pili, Lala Salama (2012).

  1. Alikiba – Aje (2017)

Sababu ya Wema kuwa anamuita Alikiba ‘Bichwa’ ilianzia katika wimbo huu, Aje (2017) ambao Kiba aliwekeza sana, mathalani video yake tu iliyofanyika Afrika Kusini iligharimu Dola32,000, wastani wa Sh75.3 milioni kwa sasa.

“Uzuri wake timilifu nishamuona na watu maarufu tu, kina Wema Sepetu nikaomba namba bichwa akanishushua shuu!” Alikiba katika ngoma, Aje ambayo ilifanya vizuri hadi Sony Music Africa kumpatia tuzo.

  1. Fid Q – Sumu (2016)

Rapa huyo mwenye albamu tatu sokoni, Vina Mwanzo Kati na Mwisho (2005), Propaganda (2009) na KitaaOlojia (2019) katika ngoma yake, Sumu kamataja Wema na Zari.

Download Music: Diamond Platnumz – Kesho

“Oyoooo time is money nafasi haijali kuzuga, Wema anataka saa ya almasi Zari anaujali muda,” Fid Q katika ngoma, Sumu ambayo pia aligusia ushindani wa Alikiba na Diamond na mtazamo wa wadau kuwahusu.

Wema Sepetu Bongofleva
  1. Harmonize – Mtaje (2021)

Ngoma hii Harmonize aliitoa kwa ajili ya aliyekuwa Mchumba wake, Kajala Masanja kipindi anambembeleza warudiane ndipo ndani yake akamtaja na Wema ambaye alikuwa ni rafiki mkubwa wa Kajala miaka nyuma.

“Nilianza kumuona mapema, enzi za mabanda ya sinema. Alikuaga ni rafiki na Wema she’s so beau, acha wanione mshamba tuu!,” Harmonize katika ngoma, Mtaji kutoka kwenye albamu yake ya pili, High School (2021).

  1. Aslay – Natamba (2017)

Baada ya kuachana na kundi la Yamoto Band na kuanza kufanya kazi pekee, Aslay alikuwa anatoa ngoma mfululizo, mmoja wapo ni hii, Natamba ambayo amemsifia Wema kwa kuwa na shepu ya kuvutia.

Soma pia Mambo 10 usiyoyajua kuhusu Hamisa Mobetto

“Aaaaae! angalia shepu, Aaaaae! ka-Wema Sepetu, Aaaaae! angalia jicho, aaaaae! Hamissa Mobetto,” Aslay katika ngoma, Natamba ambayo video yake ina ‘views’ zaidi ya milioni 14 YouTube.

  1. Joh Makini – Mchele (2019)

Rapa huyu kutoka River Camp Soldiers na Weusi, katika ngoma yake, Mchele anamtaja Wema na hasimu wake katika mitandao, Zari The Bosslady aliyempokonya Diamond wake kipindi cha nyuma.

“Tusifanye vishow so tujaze arena, tusikwame ki-Bongo, ki-Zari na Wema,” Joh Makini katika ngoma, Mchele akimshirikisha Young Lunya ambaye amesainiwa Sony Music Africa.

  1. Tundaman – Sio Demu (2012)

Licha ya Tundaman kuwa anamzungumzia mtu mwingine katika wimbo huu, Sio Demu, alilazimika kutaja jina la Wema Sepetu pamoja na warembo wengine ambao nao kwa kiasi fulani wamekuwa wakiimbwa katika Bongofleva.

“Jack Wolper au Shilole (sio, sio, sio), Wema Sepetu au Lulu (sio, sio, sio), Rose ndauka au Hamisu (sio, sio, sio)” Tundaman katika ngoma, Sio Demu ambayo Jacqueline Wolper, Shilole na Elizabeth Michael ‘Lulu’ walitokea katika video yake.

  1. Rostam – Hivi Ama Vile (2017)

Kundi hilo linaloundwa na Roma na Stamina (Rostam) katika wimbo wao, Hivi Ama Vile ambao upo katika mtindo wa majibizano, hapa kuna mmoja timu Wema na mwingine timu Zari.

“Mimi Wema wewe boya tu unalipi la kusema?” Roma anamuuliza Stamina ambaye anajibu kwa kusema, “Mimi Zari niko zangu Madale na naishi vyema” Rostam katika ngoma, Hivi Ama Vile ambayo ndio ya kwanza kuachiwa na kundi hilo.

  1. Rayvanny – Natafuta Kiki (2016)

Wimbo wake wa pili kuachia chini ya WCB Wasafi, Natafuta Kiki, Rayvanny akaona apite na Wema Sepetu pia alitokea kwenye video yake iliyoshika nafasi ya 12 katika orodha ya video za muziki zilizotazamwa zaidi YouTube Tanzania 2016.

Wema Sepetu Bongofleva

Soma pia Mambo usiyoyajua kuhusu Lady Jaydee

“Nataka nifanye sinema kwa Rosa na Ray si Wema, kiki ipi iko njema au niende kwa Sepetu Wema,” Rayvanny katika ngoma, Natafuta Kiki ambayo ilimuwezesha kuwania tuzo za MTV MAMA 2016 ingawa hakushinda.

  1. Marioo – Tomorrow (2023)

Ni wimbo ambao umeongezwa (deluxe edition) katika albamu ya Marioo, The Kid You Know (2022) na kuifanya albamu hiyo kuwa na jumla ya nyimbo 21, katika ‘Tomorrow’, Marioo kamzungumzia Wema, tena kuhusishwa kutoka naye!.

“Mara aseme natoka na Wema Sepetu, anasema natoka na Hamisa Mobetto,” Marioo katika ngoma, Tomorrow ambayo katika video yake katokea mpenzi wake, Paula ikiwa ni video ya pili kufanya pamoja baada ya Lonely.

Editor

Related Posts

Lifahamu tamasha la Met Gala

Lifahamu tamasha la Met Gala

Billnass afunguka kwanini hajataka kuajiriwa

Billnass afunguka kwanini hajataka kuajiriwa

Diamond, DJ Khaled waiga maujanja ya Madee

Diamond, DJ Khaled waiga maujanja ya Madee

Mkasa wa Hamisa Mobetto kutoswa na Diamond studio

Mkasa wa Hamisa Mobetto kutoswa na Diamond studio

error: Content is protected !!